Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-Udhma Wahid Khorasani, miongoni mwa Maraji' wakuu wa Kishia, ambaye kwa siku kadhaa zilizopita alikuwa amelazwa katika hospitali moja mjini Qom Iran, amefariki dunia muda mfupi uliopita.
Maandishi ya taarifa iliyotolewa na Ofisi yake tukufu ni kama ifuatavyo:
ِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحیمِ
إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَیْهِ رَاجِعُونَ
یا أَیَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ارْجِعِی إِلی رَبِّکِ راضِیَةً مَرْضِیَّةً فَادْخُلِی فِی عِبادِی وَ ادْخُلِی جَنَّتِی
Kwa masikitiko na huzuni kubwa, tunatangaza kifo cha faqihi wa Ahlul-Bayt (a.s.), Marji' mwenye hadhi ya juu katika ulimwengu wa Kishia, mwanazuoni mcha Mungu na mwalimu mkuu wa Hawza, Ayatullah al-Udhma Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu amrehemu).
Alikuwa faqihi mwenye daraja ya juu, ambaye baada ya miongo kadhaa ya kusoma, kufanya utafiti na kufundisha elimu za kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w.), kujitolea kutetea utukufu na heshima ya Ahlul-Bayt (a.s.), kusimamia na kuwahudumia mayatima kwa niaba ya Imam wa Zama hizi (a.j.), kulea na kuandaa idadi kubwa ya wanazuoni mahiri, pamoja na kufufua na kuhuisha alama na sherehe za kidini, hususan maombolezo ya Bibi Fatimah al-Zahra (s.a.), baada ya siku za kuadhimisha kumbukumbu ya shahada yake, ameikabidhi roho yake kwa Muumba wake.
Kifo chake kimezitia huzuni kubwa nyoyo za wote waliokuwa wakimpenda na kumheshimu kwa dhati, kutokana na mapenzi yake makubwa kwa familia ya Utume na Uimamu (a.s.).
Tunatoa rambirambi zetu kutokana na msiba huu mkubwa usioweza kufidiwa kwa hadhi tukufu ya Baqiyyatullah al-A'dham (roho zetu ziwe fidia kwake), Hawza zote, wapenzi na wafuasi wa hadhi ya Fiqhi na Maraji', pamoja na Waislamu wote wa Kishia.
Ratiba zinazohusu maandalizi ya mazishi, maziko na hafla za kuomboleza zitatangazwa baadaye.
Ofisi ya Ayatullah al-Udhma Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu amrehemu).
Maoni yako